Pages

Bunge Lamkingia Kifua Zitto Kabwe......Lasema Bado ni Mbunge Halali na Spika wa Bunge ana Mamlaka Kisheria Ya Kutengua Maamuzi ya CHADEMA


Ofisi ya Bunge imesema haijapata barua yoyote kuhusu kuvuliwa uanachama kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).

Kauli ya hiyo ya Bunge imekuja siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza kumvua uanachama Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa
Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema kutokana na hali hiyo, Zitto bado ni mbunge halali wa Kigoma Kaskazini na kwamba anapaswa kuendelea na shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
Dk Thomas Kashililah, amebainisha kuwa endapo Bunge litapata taarifa rasmi ya Chadema kumvua uanachama Zitto, lazima Bunge hilo lifanye kwanza uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili ndipo litoe uamuzi.
Pia amesema sakata la mbunge wa Bunge hilo kuvuliwa uanachama na chama chake si la kwanza, kwani tayari kuna mbunge aliyevuliwa uanachama na chama chake lakini Bunge hilo halikumvua uanachama wake baada ya kumaliza uchunguzi wake. Hata hivyo hakumtaja mbunge huyo.
“Utaratibu ulivyo, chama huliandikia Bunge kuhusu kumvua uanachama mbunge na Bunge kabla ya uamuzi wowote hufuatilia kwanza sababu za kuvuliwa uanachama huo, ili kujiridhisha kama zilikuwa halali au la,” alisema Kashililah.
Alisema baada ya hapo Bunge hilo huwasiliana na Msajili wa Vyama vya Siasa ili ofisi hiyo ya msajili iweze kupitia Katiba ya chama husika na kupitia sababu za chama husika zinazoweza kumvua uanachama mwanachama wake na kama kweli zimekiukwa.
“Baada ya suala hilo kupelekwa kwa msajili wa vyama vya siasa, Spika wa Bunge, hutoa uamuzi baada ya kuchunguza na uamuzi huo, hupelekwa kwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kwa ajili ya kufanyiwa kazi zaidi,”alisisitiza.
Aidha alisisitiza: “Si lazima Spika akubaliane na uamuzi wa kutengua ubunge wa mbunge husika kwani kama haikuwa halali kwa mbunge huyo kuvuliwa uanachama, Spika hubatilisha uamuzi wake wa kumvua ubunge mhusika,” alisema.
Alisema Spika Anne Makinda katika kipindi chake alishawahi kutoa uamuzi wa kubatilisha mbunge fulani kuvuliwa ubunge hata baada ya chama chake kumvua uanachama.
Akizungumzia suala hilo, Zitto, alisema kwa upande wake bado ni mbunge na anaendelea na kazi yake ya Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) hadi pale atakapopatiwa taarifa rasmi ya kuvuliwa uanachama na ubunge wake.
“Naendelea na kazi kama vile hakuna kilichotokea, sina taarifa yoyote ya kuvuliwa uanachama wangu wala ubunge, habari hizi nimezisikia kwenye vyombo vya habari, sijaitwa na Mahakama kuambiwa kinachoendelea,”alisema Zitto.
Alisema kwa sasa anaendelea kuongoza kamati hiyo na jana alikutana na menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), leo kamati yake inatarajia kukutana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pia watakutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mwanasheria Mkuu kuhusu mapato ya akaunti za madini.
Aidha alisema pamoja na kuendelea kama kawaida na shughuli zake za kibunge bungeni, pia anatarajia kesho kwenda Kigoma kwa ajili ya shughuli za maendeleo jimboni kwake, kabla ya kuhudhuria vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza rasmi Machi 17, mwaka huu.
Alisema kwa upande wake, anachukulia suala hilo kama changamoto ambayo inazidi kumkuza na kumkomaza katika medani za siasa nchini na duniani kote.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema chama hicho kinajitahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa kuzingatia sheria na taratibu zote, ikiwemo kuandaa na kuiwasilisha wakati wowote barua inayomvua uanachama Zitto, ili suala hilo lifanyiwe uamuzi mapema.
“Kwa sasa suala hili la Zitto limewaingia Watanzania wengi, sasa sisi tunataka tulifanyie kazi mapema, ili uamuzi ufanywe mapema na suala hili liishe. Kuna mambo mengi ya maana yanahitaji kujadiliwa kitaifa kama vile masuala ya uandikishaji katika Daftari la Wapiga kura kwa mfumo wa BVR,” alisema.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye juzi alitangaza kuwa chama hicho kimemvua uanachama mbunge huyo, jana alimwambia mwandishi kuwa, jopo la wanasheria wa chama hicho litaifikisha taarifa ya Zitto kuvuliwa uanachama kwa Kamati Kuu ya chama ifikapo Mei, mwaka huu.
Alisema, "Kutokana na utaratibu uliopangwa wa Kamati Kuu kukutana kila baada ya miezi mitatu, suala la Zitto litasubiri kikao kingine cha kawaida cha kamati hiyo kitakachokaa mwezi Mei. Kikao kilichopita kilikaa Februari mwaka huu".
Kwa maelezo ya Lissu, baada ya hapo ndipo wataiandikia barua Tume ya Uchaguzi (NEC) kuijulisha kuwa Zitto si mwanachama wa chama hicho tena au la.

5 comments: